TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE “DENGUE FEVER”
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa Umma juu ya
mwenendo wa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue fever” hapa
nchini.Ugonjwa huu umethibitishwabaada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka
kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es Salaam kupelekwa
kwenye maabara yetu ya Taifa Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na
virusi vya homa ya dengue mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014. Hadi
sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huuni 400 na
Vifo 3. Kwa wiki iliyoshia tarehe 9 Mei 2014 ya idadi ya wagonjwa
waliogundulika mkoani Dar es salaam ni 60 (42-Kinondoni, 14-Temeke na
4-Ilala) na idadi ya wagonjwa waliopo wodini mpaka sasa ni 13.
Aidha, mlipuko wa ugonjwa huu si mpya hapa nchini kwani uligundulika kwa
mara ya kwanza mnamo Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu
40 walithibitika kuwa na ugonjwa. Pia, kati ya mwezi Mei hadi Julai
2013,wagonjwa 172 walithibitishwa kuugua ugonjwa huu.
Homa ya Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dengue in ugonjwa uliosambaa duniani katika nchi za ukanda wa joto.
Takribani asilimia 40 ya watu wote duniani wanaishi katika nchi zenye
ugonjwa huu. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinathibitisha kuwa
takribani matukio milioni 5 ya Dengue yanatolewa taarifa kila mwaka.
Watu laki 5 hulazwa hospitali kwa kuathirika na Dengue kali. Homa ya
Dengue imeshatokea katika nchi zipatazo 34 barani Afrika.
Hapa Afrika Dengue ni ugonjwa unaojulikana kwa kiwango kidogo sana.
Licha ya kwamba milipuko ya kwanza imetokea tangu mwanzoni wa karne ya
19. Matukio ya Ugonjwa huu yameongezeka Afrika tangu miaka ya 1980,
matukio mengi yakitokea nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ikiwa ni
pamoja na Msumbiji, Somalia, Kenya, Komoro, Djibouti na Tanzania.
Ikumbukwe kuwa jina “Dengue” linatokana na neno “Dinga” la kiswahili
linalolomaanisha ugonjwa unaotakana na pepo yaani Kudinga pepo.
Mabaharia wa Kispanish walipokuja kwenye pwani ya Afrika Mashariki
walirudi kwao na kuuita “Dengue”.
Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na
uchovu Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia katisiku ya 3 na 14 tangu
mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue. Kwa wakati mwinginedalili
za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi
wananchi wanaombwa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima ili
kugundua kama wana vimelea vya malaria ua la ili hatua stahiki
zichukuliwe.
Kuna aina 3 tofauti za namna ugonjwa huu unavyoweza kujitokeza iwapo mtu aking`atwa na mbu mwenye virusi hivi;
i.Homa ya dengue (Dengue Febrile Illness): Aina hii huambatanana dalili
kuu tatu za homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au
uchovu.Aidha, kwa Tanzania mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa
wamejitokeza na dalili hizi.
ii.Dengue ya damu (Dengue Haemorrhagic Fever): Aina hii yahoma ya dengue
huambatana na dalili za mgonjwa kutokwa na damu kwenye fizi au puani,
vile vile kutokwa na damu chini ya ngozi.Iwapo mgonjwa huyu ataumia
sehemu yoyote ni rahisi kwake kupoteza damu nyingi kupitia kwenye
michubuko.
iii.Dengue ya kupoteza fahamu (Dengue Shock syndrome): Aina hii ya homa
yadengue huambatana na mgonjwa kupoteza damu nyingi ambayo hupelekea
mgonjwakupoteza fahamu. Dalili hizi zimeonekana kwa mgonjwa 1 kati ya
wagonjwa 400 waliokwisha kuthibitishwa kuwa na ugonjwa hapa nchini.
Kirusi cha homa ya Dengue kinaambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine
kwa kuumwa na mbu wa Jamii ya Aedes, na hasa Aedes aegypti. Mbu huyu
anaishi katika mazingira ya makazi ya binadamu. Huuma wakati ya mchana
ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli, hususani majira ya
asubuhi na jioni kabla jua halijazama.
Mbu huyu anazaliana katika maji yaliyotuama hasa kwenye vyombo vya
nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba, matairi ya gari, ndoo, vikopo,
na kadhalika. Kwa bahati mbaya mbu huyu huweza kuzaliana katika vifaa
vidogo vidogo ambavyo watu wengi huvidharau. Hivi ni pamoja na makopo ya
kuotesha maua, vikombe, vifuu vya nazi, na kadhalika. Majani mapana
yanayohifadhi maji ni mazingira mazuri kwa kuzaliana kwa mbu huyu, hivyo
maeneo ya bustani siyo ajabu kuwa mahali pazuri kwa mbu hawa.
Ugonjwa huu hauambukizi kwa kumhudumia mgonjwa au kugusa majimaji
yanayotoka kwa mgonjwa. Homa ya dengue inaweza kutibika kama mgonjwa
atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.Hakuna dawa
maalumu ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana nadalili
zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au
damu. Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza
kupoteza maisha.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
Kuangamiza mazalio ya mbu
Fukia madimbwi ya maji yaliyotuamaau nyunyuzia viuatilifu vya kuua viluwiluwivya mbu kwenye madimbwi hayo
Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile: vifuu vya
nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
Funika mashimo ya maji takakwa mfuniko imara
üSafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama
Kujikinga na kuumwa na mbu
Tumia viuatilifu vya kufukuza mbu “mosquito repellants”
Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
Tumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa wale wanaolala majira ya mchana na hasa kwa watoto)
Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Hatua zinazochukuliwa na Wizara
(i)Hatua za Dharura
Uratibu
Timu ya Taifa ya Maafa inayoshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wa
Halmashauri za Jiji na Wadau wa Maendeleo hukutana kila mara 2 kwa wiki
kutathmini mikakati ya dharura iliyowekwa.
Uelemishaji na Uhamasishaji wa Jamii
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitoa tamko la Serikali kwa nyakati
tofauti kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Dengue. Tamko la kwanza lilitolewa
kwenye vyombo vya habari tarehe 04 Februari 2014 na Machi 2014.
Kuendelea kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga
Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara. Aidha taarifa hii pia
iinajumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa),
“Ukweli Kuhusu Ugonjwa“(Fact sheet), Mwongozo kwa watumishi wa afya wa
namna ya kuchukua sampuli. Vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga
na maambukizi ya ugonjwa huu vitatolewa.
Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia Radio, na Runinga. Aidha
Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za jiji wameendelea kutumia
Maafisa Afyaikiwemo wa kata kuwaelemisha wananchi namna ya kudhibiti
ugonjwa kwakutumia vipaza sauti, uongozi wa mitaa
Mafunzo kwa watalaam wa Afya
Kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa Watumishi wa Afya ikiwa pamoja na
madaktari na mafundi maabara namna ya kutambua ugonjwa huu. Aidha
watumishi wa hospitali za Muhimbili, Mwananyamala, Amana na Temeke
wamekwisha kupewa mafunzo haya na bado wanaendelea kupewa kupitia
mikutano yao ya asubuhi (Clinical meetings). Mafunzo haya pia
yanaendelea kutolewa kwa vituo vya chini kupitia Halmashauri
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na mawasiliano
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma za
afya pamoja na mipakani kupitia mfumo wa saveilensi ya Wizara. Aidha,
pamoja na Mwongozo huu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa
maelekezo kwa Waganga wakuu wa mikoa na wilaya hapa nchini kutoa taarifa
za wagonjwa wa Dengue Fever kupitia taarifa za kila juma.
Kutoa miongozo ya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika maeneo ya mipakani
kuhusu kutokuwepo kwa aina yoyote ya vikwazo vitakavyowekwa kwa ajili
kwa wasafiri. Aidha maelekezo hayo yameainisha kuwa iwapo msafiri
anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa
watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa
Kufuatilia kwa karibu ongezeko la wagonjwa wenye homa isiyo kuwa ya
malaria kwa Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya uchunguzi wa
kina iwapo kuna ugonjwa huu. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
imeshafanya utafiti mkoani Kagera, Morogoro na Kigoma na kuthibitisha
kuwa haijaadhirika na dengue.
Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika
Hospitali za Manispaa za jiji la Dar es Salaam (Mwananyamala, Amana na
Temeke). Aidha, Kituo cha ‘International School of Tanganyika – IST’
kilichopo Manispaa ya Kinondoni na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
zinaendelea na ufuatiliaji wa ugonjwa huu. Aidha Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii itafungua pia vituo mkoani Tanga na Mtwara, mikoa
imayopakana na nchi jirani yaani Kenya na Msumbiji ambako ugonjwa huu
pia umetolewa taarifa.
·Kupeleka taarifa ya mlipuko huu Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kama mwongozo wa Kanuni za Afya za Kimataifa uvyaoelekeza.
Upimaji na Tiba
Kuimarisha uwezo wa kutambua ugonjwa huu kwa kina kupitia maabara ya
Taifa (NHLQATC) iliyopo NIMR. Vile vile Wizara imepeleka vipimo sawia
yaani “Dengue Rapid Test Kits” kwa vituo vya Dar es Salaam kuimarisha
utambuzi. Vituo hivo ni pamoja na hospitali za Muhimbili, Amana,
Mwananyamala, Temeke Hospital, na IST kliniki. Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii imeagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuhakikisha vitendanishi hivi
vinakuwepo ili kurahisisha upatikanaji wake kwa Halmashauri zote na
kupelekwa kwenye vituo vya chini zaidi. Wizara imeagiza vipimo sawia 750
vya kunyongeza ambavyo tunatarajiwa kuvipata tarehe 22.5.2014
Wizara imeweka utaratibu wa kuhakikisha vifaa Tiba vinapatikana wakati
wote katika vituo vyote kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa
watakaogundulika na kuwa na ugonjwa huu.
Udhibiti wa mbu na mazalia
Kudhibiti mbu kupitia kwa kupulizia na kunyunyizia viuatilifu katika
baadhi ya maeneo yaliyoathirika katika mkoa wa Dar es salaam ambayo
wametoka wagonjwa wengi wa Dengue. Hii inalenga kuangamiza mbu wapevu na
viluwiluwi.
Utafiti
Taasisi ya Utafiti ya magonjwa ya Binadamu (NIMR) iko katika maandalizi
ya kufanya utafiti kuhusu dengue kwa kuangalia maaeneo makubwa mawili.
Ukubwa wa tatizo katika binadamu
Mbu waambukizao ugonjwa wa homa ya Dengue- kujua jamii husuka, tabia ya
kuuma watu, wapi wanapopendelea kuuma, wapi wanakozaliana kwa wingi na
mazingira yao ya kawaida.
Tafiti hizi zinaanzia Dar es Salaam na kuhusisha wilaya zote tatu
(Ilala, Kinondoni, Temeke). Tafiti zitaendelea katika baadhi ya mikoa,
ikiwa ni pamoja na mikoa 8 ambako vituo vyetu vipo.Takwimu
zitakazopatikana zitaboresha mbinu za kupambana na ugonjwa huu
(ii)Hatua za Kudumu
WAUJ imeandaa Mpango wa wa namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Homa ya Dengue. Mpango huu kwa kushirikisha sekta mbalimbali.
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa Dengue
Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu kwani
hauambukizwi kwa kumhudumia mgonjwa au kwa kugusa majimaji yanayotoka
kwa mgonjwa. Hata hivyo tunawashauri wananchi kwenda kwenye vituo vya
afya haraka pindi wanonapo dalili za ugonjwa huu.
Mlipuko wa Dengue unadhihirisha kuwa mazingira yetu tunayoishi si
salama. Ikumbukwe kuwa, kwa sehemu kubwa, ugonjwa huu unachochewa na
mazingira machafu. Aidha mvua hizi kubwa zinazoendelea zonachangia
kuongezeka kwa mazalio ya mbu. Utupaji, uzoaji na uhifadhi wa taka
katika miji yetu hauridhishi kiasi ambacho kinatoa fursa kwa mazalio ya
mbu kuongezeka na hata kuwa karibu zaidi ya makazi ya binadamu.
Kwa kuwa, hadi sasa hakuna chanjo wala dawa maalumu kwa ajili ya
kudhibiti au kutibu ugonjwa huu, njia kubwa ya kupambana na ugonjwa huu
ni kumzuia binadamu asimwe na mbu. Hivyo basi, mbinu shirikishi za
kutokomeza mbu inabidi zitiliwe mkazo katika mapambano dhidi ya homa ya
Dengue. Njia bora na rahisi ni kuhakikisha mazalio yote ya mbu
yanatokomezwa. Na hili laweza kufanywa na kila mtu kwa nafasi
yake.Tunashauri watu wavae nguo zinazofunika mikono na miguu na dawa
zinazofukuza mbu (mosquito repellent). Tunaelewa kuwa si kila mtu
atakuwa na uwezo wa kununua dawa hizi na ndiyo maana tunakazania swala
la kuangamiza mazalia ya mbu ambalo ni jukumu letu wote.Tunaendelea
kuhamisisha watu na hasa watoto walale ndani ya vyandarua venye
viatilifu wanapolala wakati wa mchana.
Ningependa kuwakumbusha wananchi wa Tanzania kuwa, huu ni muda muafaka
wa kuzingatia utunzaji bora wa mazingira yetu. Tukitunza mazingira yetu,
nayo yatatutunza na kutuepusha na maradhi yanayoambatana na mazingira
machafu.
Charles A. Pallangyo
Katibu Mkuu
12 May 2014
Post a Comment
LEAVE YOUR COMENT HERE...